Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa wito kwa Wabunge kutenga rasilimali zaidi kwa wizara ya Michezo.

Wetang’ula alisema riadha bila shaka ndicho chombo nambari moja cha kuitangaza Kenya kimataifa.
Akizungumza katika Kaunti ya Uasin Gishu siku ya Jumamosi asubuhi, Spika Wetang’ula alisema Wimbo wa Taifa la Kenya umekuwa ukipigwa katika miji mikuu ya kimataifa kutokana na juhudi, ustahimilivu na nia ya wanariadha wa nchi hii.
Akihutubia wanariadha katika toleo la tatu la Great Chepsaita Cross Country Run, Wetang’ula alisema Kenya ina vipaji visivyo na mipaka.
“Tunajivunia kila mara tunapoona wanamichezo wetu wakiume na wa kike wakishinda mbio katika ulingo wa kimataifa. Kila ninapoona vijana wetu wakishinda katika majukwaa ya kimataifa, najivunia zaidi kuwa Mkenya.”
Tukio hilo la kila mwaka linaandaliwa na Msaidizi Binafsi wa Rais William Ruto, Farouk Kibet.
Wetang’ula alimpongeza Farouk kwa hatua hiyo nzuri ambayo imeipa nafasi vipaji kukuzwa katika makundi mbalimbali ya umri.
“Katika nafasi yangu kama Spika wa Bunge la Taifa, nahimiza Wabunge kutenga rasilimali zaidi kwa michezo ili kukuza vipaji. Nitajitolea kila mara kuunga mkono shughuli za michezo.”
Spika alisisitiza: “Lazima tupendane na kumuunga mkono Rais Ruto na Serikali yake ili kuhakikisha uongozi unatimia malengo yake. Vipaji vyetu havina mipaka na vitatupeleka mahali tunapaswa kuwa. Sote lazima tujivunie kuwa Wakenya.”
Gavana wa eneo hilo Jonathan Bii alisema uongozi wake utaendelea kuunga mkono shughuli za michezo.
“Tumeona vijana wakishiriki shughuli mbalimbali za michezo. Ni heshima kuwa na watu kama hawa na tuna uhakika wa mustakabali mzuri katika michezo.”
Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alisema atazindua toleo lingine la tukio hilo ili kuendeleza vipaji kote nchini.
“Mratibu ametonyesha njia; tutafuata nyayo. Huu ni hatua kubwa katika shughuli za michezo nchini,” aliongeza.
Katibu Mkuu wa Elimu ya Msingi Profesa Julius Bitok alisema tukio hilo linaendelea kulea vipaji kote nchini.
“Serikali imefanya mengi katika sekta ya Elimu. Najivunia kwamba tukio la leo limepangwa mahsusi kuunga mkono masuala ya Elimu.”
Bingwa wa dunia wa riadha Paul Tergat alisema tukio hilo linawatia motisha wengi wanaotaka kujipatia kipato kupitia michezo.
“Tutakuwa na vipaji vingi siku zijazo. Wadau wote wanapaswa kukumbatia wazo kwamba vijana wetu wanaweza kushiriki kikamilifu katika michezo,” alisema Paul.
Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nandi, Muge Cynthia, alitoa wito wa kujumuishwa kwa uongozi wa nchi katika shughuli za michezo.
“Tunajivunia kama Taifa kwamba tumetambuliwa duniani kutokana na vipaji. Sote lazima tushikamane tusipoteze vipaji hivi vikubwa,” aliongeza.

